NewsSWAHILI NEWS

Arusha waua wanne wakidaiwa kuiba kuku, simu

Arusha. Watu wanne wamefariki dunia jijini Arusha katika matukio mawili tofauti baada ya kushambuliwa na wananchi wenye hasira kwa tuhuma za wizi.

Watu hao wameuawa alfajiri ya leo Julai 11, 2024 wakiwemo wawili waliopigwa na wananchi katika kata ya Muriet kwa tuhuma za wizi wa kuku na wengine wawili wakiuawa kwa tuhuma za uporaji wa simu.

Katika tukio la kwanza lililotokea Kata ya Murieti, watu wawili wamefariki dunia baada ya kukamatwa wakidaiwa kuiba kuku.

Wakizungumza katika eneo la tukio, shuhuda wa tukio, Ally Rajabu amesema saa 11 alfajiri alisikia kelele la mwizi, mwizi, mwizi, zikitokea barabarani na alipochungulia dirishani aliona watu wengi wakikimbia huku wawili wa mbele wakiwa wamebeba kuku.

“Ile nimekaribia kundi kubwa likawazunguka wale watu wawili na kuku mkononi na kuanza kuwapigwa. Kila mtu alitumia silaha aliyokuja nayo huku wengine wakiwaponda kwa mawe makubwa yaliyokuwa karibu na eneo la hilo hadi mauti yalipowafika,” amesema Ally.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Murieti, Emmanuel Sanare amesema alipigiwa simu saa 12 asubuhi na mmoja wa wananchi akitakiwa kufika eneo la tukio kushuhudia wezi, lakini alipofika alikuta tiyari watu hao walishafariki.

 “Mimi nilikuta watu walishafariki, ingawa kuna watu waliokuwa wakizidi kuja na kutaka kumalizia hasira zao kwa kupiga hata maiti, hivyo tuliingia kibarua cha kuzuia ili angalau waweze kutambuliwa lakini hali ilikuwa sio rahisi,”amesema Sanare.

Naye Aisha Rashidy amesema kuwa alishuhudia watu hao wakipigwa huku wameshika kuku mikononi mwao hadi wakaishiwa nguvu na wakawaachia huku wakiomba kusamehewa bila mafanikio kutokana na wananchi kuwa na hasira.

“Watu wamefikia hatua hii kwa sababu wamechoka kuibiwa, kila siku wanaiba kuku mitaa hii, wanavunja nyumba, wanapora vitu usiku na ukikaa vibaya wanaweza hata kukuua,” amesema.

Amesema wengi wanaoiba ni wale wanaotembea mchana majumbani wakijifanya waziba mabeseni na ndoo au wananunua vyuma chakavu, kumbe wanasoma ramani ya nyumba ilivyo.

“Usiku wakija wanajua cha kuchukua na kwa kuku wanawapulizia dawa ya mbu au yoyote ya kulevya, wanalegea na kuchukuliwa kirahisi bila kupiga kelele, kisha wanawatumbukiza kwenye mfuko wa salfeti na kuondoka nao kwenda kuchinja na kuuza masokoni,” amesema Aisha.

Katika tukio lingine, watu wengine wawili waliokuwa wamepakizana kwenye bodaboda wameuawa kwa kipigo na wananchi katika jaribio la kutaka kukimbia baada ya kudaiwa kupora simu katika Kata ya Kaloleni jijini Arusha.

Mbali na watu hao kuuawa pia pikipiki waliyokuwa nayo imechomwa moto.

Wakizungumza katika eneo la tukio, mmoja wa mashuhuda Lilian Shayo amesema asubuhi ya saa moja, watu hao wakiwa na pikipiki walionekana wakimpiga kaka mmoja kikumbo na kupora simu yake, lakini katika jaribio la kutaka kukimbia waliwekwa kati na kuanza kushushiwa kipigo.

“Haya matukio ya wizi yamekuwa yakitokea sana, tena wakidaka kitu wanachotaka kuiba kama pochi, simu au kitu cha thamani, ukiking’anga’ania wanakuchoma kisu cha mkono au shingo, ukiachia wanachukua wanaondoka,” amesema.

Naye William Shayo, amesema katika tukio hilo wananchi wamechoma pikipiki na wakati wakiwa katika harakati za kuwachoma watuhumiwa baada ya kuuawa, polisi waliokuwa doria walifika na kuwaokoa kuondoka nao.

 “Arusha watu wamechoka na maisha, jua kali, migogoro ya kila kukicha, familia zetu ni shida, lakini pia wizi wa vijana wadogo unatutesa, ndio maana kila wakikamatwa sasa hivi wanauawa kama hivi, hivyo niwaombe vijana wenzangu watafute tu kazi za kufanya, sio kuombaomba wala kuiba,” amesema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha SACP Justine Masejo amesema hakuwa na taarifa za undani za matukio hayo na kuwa waliouawa hawakuwa wametambuliwa.

“Tumehifadhi miili katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali yetu ya Mount Meru kwa utambuzi wa maiti kutoka kwa ndugu au jamaa zao,” amesema Masejo.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!