NewsSWAHILI NEWS

Adhabu ya viboko 70 ilivyosababisha kifo cha kijana wa kimasai

Arusha. William Mollel ‘Rasta’ (35), mkazi wa Jijini Arusha amefariki dunia baada ya kupewa adhabu ya kimila ya kuchapwa viboko 70 iliyotolewa na wazazi wake kwa kosa la kuitelekeza familia yake.

Adhabu hiyo iliyotolewa juzi Julai 7, 2024, imeelezwa hutolewa na wazee wa jamii ya kimasai na kimeru mkoani Arusha kwa vijana wao wanaobainika kufanya matendo ambayo ni kinyume cha maadili.

Miongoni mwa matendo hayo ni pamoja na kutukana wazazi, kunywa pombe mchana na kufanya vurugu, kuvaa nguo zisizo za heshima na kufanya uhalifu ikiwemo kupigana.

Tukio hilo limetokea takribani mwaka mmoja tangu Nelson Mollel (32), mkazi wa Sanawari, wilayani Arumeru, Arusha afariki dunia mwaka 2023, baada ya kudaiwa kupewa adhabu ya kuchapwa vikobo 280 kwa tuhuma ya kumtukana mama yake mzazi.

Rasta  aliyekuwa akiishi jijini Arusha, inaelezwa alichukuliwa na familia yake Julai 7, 2024 na kupelekwa nyumbani kwao katika kijiji cha Orkeswa, wilayani Monduli kwa ajili ya kikao kuhusu kosa la kutelekeza familia yake. Kikao hicho kiliamua aadhibiwe kwa kuchapwa viboko 70.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Orkeswa, John Meng’oriki Laizer akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Julai 9, 2024 kuhusiana na tukio hilo, amesema alipewa taarifa kuwa Rasta ametelekeza mke na mtoto kwa mama yake mzazi kijijini na kuhamia mjini.

Amesema huko alioa mke mwingine na siku ya tukio walitumwa watu wakamdanganye kwamba anahitajika kwenye kikao cha familia.

“Walipofika naye kikaoni ndiyo ikaamriwa adhibiwa kuchapwa viboko 70. Saa 12 jioni alirudishwa nyumbani akiwa hoi na saa mbili usiku siku hiyo hiyo akafa,” amesema mwenyekiti huyo.

Laizer amesema baada ya tukio hilo, wasamaria wema walitoa taarifa polisi ambao walifika haraka nyumbani hapo, lakini hawakumkuta mtu zaidi ya mwili wa marehemu ulioachwa ndani ya nyumbani.

“Polisi walibeba ile maiti na kuondoka nayo na baadhi ya watu walikamatwa na wengine walikimbia,” amedai Laizzer.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo, amesema watu watatu, akiwemo baba na ndugu wengine wa familia hiyo, wanashikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.

“Bado tunaendelea na upelelezi wa tukio hili, ikiwemo kuwasaka wengine wanaodaiwa kuhusika. Ikithibitika wamehusika, sheria itachukua mkondo wake dhidi yao, kwani tayari tukio la mauaji ni jinai,” amesema Masejo.

Mamile Ole Ikururu, mmoja wa viongozi wa kimila wilayani Monduli, amesema adhabu hizo zilipitishwa zamani kwa lengo la kurudisha maadili na nidhamu kwenye jamii.

Hata hivyo, kutokana na hali ya afya ya watu, adhabu hizo zinapendekezwa kubadilishwa na kuwa faini ya mifugo pekee.

Akizungumzia hilo, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Festo Kiswaga amesema adhabu za kimila ni kubwa na zinahitaji kubadilishwa.

Amesema elimu inatolewa kwenye mikutano mbalimbali, ili kuachana na adhabu hizo, lakini baadhi ya watu wameweka pamba masikioni.

Hata hivyo, ameonya wote wanaoendelea kutoa adhabu hizo zinazoleta madhara kwa jamii kwamba watakumbana na mkono wa sheria.

“Kama hawabadiliki, tutawabadilisha kwa sheria,” amesema Kiswaga.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa Kagera linaendelea na uchunguzi kuhusu mwalimu anayedaiwa kumchapa mwanafunzi na kumjeruhi, akimtuhumu kukataa kusoma somo la fizikia.

Kamanda wa Polisi Mkoa Kagera, Blasius Chatanda amethibitisha kushikiliwa kwa mkuu huyo wa Shule ya Sekondari Kiteme, Charles Mukaluka, iliyopo Kata Kasharunga Wilaya Muleba.

Amesema Mukaluka anashikiliwa kwa tuhuma ya kumshambulia Finileth Augustine (18), mwanafunzi kidato cha tatu, huku akimshulutisha kusoma somo la fizikia.

Chatanda amesema uchunguzi wa awali unaonyesha mwalimu huyo alitumia hasira kumuadhibu mwanafunzi huyo.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha mwalimu alitumia hasira kumuadhibu mwanafunzi wake hadi kumsababishia majeraha makubwa kwenye mwili wake, lakini hakuna sheria inayoelekeza kutoa adhabu kiasi hicho,”amesema.

Hata hivyo, kaimu mganga mfawidhi wa kituo hicho cha afya Kimeya, Dk Erasto Mosha amesema Finileth ameruhusiwa kurudi nyumbani kutokana na afya yake kuimarika.

“Tumemruhusu mwanafunzi huyo kutokana na kuona anaendelea vizuri,” amesema.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!