NewsSWAHILI NEWS

ADC kufanya maridhiano na Doyo, hatima kujulikana Ijumaa

Dar es Salaam. Hatima ya aliyekuwa mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Chama cha Allience for Democratic Change (ADC), Doyo Hassan Doyo, kujulikana ndani ya siku tano kuanzia sasa, huku njia ya upatanisho ikipewa nafasi kubwa.

Hatua hiyo imetangazwa leo Jumatatu Julai 8, 2024 na kamati ya rufaa ya chama hicho ilipozungumza na waandishi wa habari ambapo pia Doyo alihudhuria mkutano huo, lakini hakuruhusiwa kuzungumza chochote.

Juni 29, 2024  chama hicho kilifanya uchaguzi mkuu wa nne wa viongozi wake na Shaban Haji Itutu, alitangazwa kuwa mshindi wa nafasi ya uenyekiti kwa kupata kura 121 dhidi ya 70 alizopata Doyo.

Baada ya matokeo hayo (siku mbili baadaye), Doyo alitangaza kukata rufaa kwenye kamati ya rufaa ya chama hicho, akipinga uchaguzi kwa madai ya kutoridhika na matokeo hayo.

Katika rufaa hiyo pamoja na mambo mengine, Doyo ameituhumu kamati ya uchaguzi pamoja na mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Hamad Rashid Mohamed kwa kukiuka katiba na kanuni za chama hicho katika uchaguzi huo.

Ilichosema kamati ya rufaa

Akimwakilisha mwenyekiti wa kamati hiyo, Charles Kitima, Said Miraji ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo, amesema katika kushughulikia rufaa hiyo, wameona waanze kwanza na upatanisho, kabla ya kusikiliza malalamiko na wamejipa siku tano wawe wamemaliza kazi hiyo.

“Kwa kuwa pande zote mbili waliridhia suala la kufanya upatanishi kwa maslahi mapana ya chama cha ADC, hivyo tunawatangazia rasmi kwamba sasa tupo katika mazungumzo na pande zote mbili kwa ajili ya kumaliza suala hili ndani ya chama,” amesema Miraji ambaye amewahi kuwa mwenyekiti wa kwanza wa  chama hicho.

Sababu zilizochangia kuanza na maridhiano, amesema kuwa ni kutambua uwepo wa Mwenyezi Mungu na viongozi kuwa nafasi kubwa ya kuwa waaminifu, waadilifu na wenye huruma kwa wanaowaongoza.

Sababu nyingine ni maridhiano kuwa moja ya misingi ya sera tisa ya chama hicho.

“Falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan ya R4, yaani maridhiano, ujenzi mpya wa Taifa, mageuzi na ustahimilivu nayo ndio inatusukuma kufanya hivyo,” amesema Miraji

Aidha, amesema historia  na desturi za kiafrika kwa kile alichoeleza hata mababu zamani hawakuwa na Mahakama, bali walitumia vikao na mazungumzo kama njia sahihi ya kutatua matatizo bila uwepo wa makovu.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!